Petr Cech Kustaafu Soka la kimataifa

Petr Cech amekiri kuwa anafikiria kustaafu soka la kimataifa kwa nchi yake Jamhuri ya Czech na kuelekeza nguvu zake kwa klabu yake ya Arsenal.
Cech amekuwa sehemu ya kikosi cha kwanza cha Czech tangu 2002 na alikuwa nyota wa timu iliyotinga nusu fainali ya Euro 2004, na kuwa kipa bora wa michuano hiyo.
Alipewa kitambaa cha unahodha mnano 2007 na amefanikiwa kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa Czech kwa mara ya nane mwezi huu.
Hata hivyo wakati michuano ya Euro 2016 ikiwa inakaribia, nyota huyo wa Gunners amekiri kuwa huenda ikawa michuano yake ya mwisho ya kimataifa.
“Natimiza miaka 34 na ni wakati wangu kuliangalia swala hili,” alisema kupitia tovuti yake.
“Nilikaa nikawaza, Je! Baada ya miaka 14 kwenye timu ya taifa, huu si ni muda muafaka kufunga ukurasa huu?
“Ingawa ni mapema  kusema hivyo, lakini nahesabu siku.
“Jinsi nitakavyo safiri sehemu mbali mbali na timu yangu ya taifa, ndivyo nitakavyoshindwa kuitumikia vema Arsenal.
“Pamoja na yote, umri wangu haurudi nyuma, naendelea kuzeeka.
“Najisikia mwenye nguvu, lakini mambo hayajabadilika tangu 2002 – nimekuwa nikisafiri sana bila kupata nafasi ya kupumzika.
“Inafikia hatua katika maisha unafikiria kufikia mwisho wa taaluma na kuchagua uelekeo mpya, uamuzi huo utakuja baada ya Euro.”

Comments