MJADALA WA VIONGOZI KUHUSU NYUKLIA
SATURDAY, APRIL 2, 2016
Obama awaita viongozi wa dunia kujadili nyuklia

Rais wa Marekani, Barack Obama.
Washington, Marekani. Viongozi zaidi ya 50 wa mataifa na Serikali pamoja na wawakilishi wa mashirika kadhaa ya kimataifa wanakutana mjini Washington kuzungumzia usalama wa nyuklia.
Hofu ya kutokea mashambulio ya kigaidi kutokana na kuibiwa vifaa vya nyuklia na kutapakaa silaha hizo ndiyo chanzo cha mkutano huo ulioitishwa na Rais wa Marekani, Barack Obama.
Pia, kitisho cha nguvu za nyuklia za Korea Kaskazini ni miongoni mwa mada zinazojadiliwa kwenye mkutano huo. Kabla ya mkutano huo kuanza, Rais Obama alizungumza na Rais Park Geun Hye wa Korea ya Kusini na Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe.
Mwishoni mwa mazungumzo hayo, Rais Obama alizungumzia umuhimu wa ushirikiano katika sekta ya usalama pamoja na nchi hizo mbili za Asia.
Rais Obama alikutana pia na Rais wa China, Xi Jingping na kuzungumzia ushirikiano wa nchi hiyo na Korea ya Kaskazini. Lengo ni kuhakikisha Korea haina kabisa silaha za nyuklia.
Jana, wajumbe kwenye mkutano huo watajadili namna ya kuendeleza mapambano dhidi ya wanamgambo wa Dola la Kiislamu (IS).
Katika hatua nyingine, wanajeshi wa Korea Kusini wamesema Korea Kaskazini imefyatua kombora la masafa marefu katika eneo lao la pwani ya mashariki ndani ya bahari, huku kikao kuhusu usalama wa nyuklia kikiendelea mjini Washington.
Ufyatuaji wa kombora hilo Korea Kaskazini ni mwendelezo wa matukio yanayofanywa na taifa hilo jambo ambalo linapingwa.

Comments
Post a Comment